Ushabiki wa madhehebu unapelekea huku

Mnajua kuwa siku si mbali sana katika Msikiti Mtakatifu wa Makkah kulikuwa Mihraab nne. Kila dhehebu linaswali mkusanyiko, Jamaa´ah yao pamoja na watu wa madhehebu yake pembezoni mwa Ka´bah. Hali iliendelea hivo mpaka hapo Allaah alipofanya kupatikana mtu ambaye aliwakusanya wote kuswali nyuma ya imamu mmoja na muonekano huu mbaya ukawa umeisha na himdi zote ni za Allaah. Yote haya sababu yake ni kufuata mambo ya madhehebu na maoni. Walitofautiana mpaka katika swalah na ikawa Hanafiy haswali nyuma ya Hanbaliy na Hanbaliy haswali nyuma ya Shaafi´iy! Isitoshe jengine ni kwamba hawaswali katika wakati mmoja ambapo wamoja wanaswali mwanzoni mwa wakati na wengine wanaswali mwishoni mwa wakati! Kwa sababu fulani anaonelea lililo la sawa ni kuchelewesha swalah na mwingine anaonelea sawa ni kuitanguliza. Wanachotaka ni kuwaridhisha watu wote! Mambo haya tumeyaona katika baadhi ya miji mingine mpaka hii leo yapo. Mpaka Ijumaa hawaswali kwa wakati mmoja. Baadhi yao wanaiswali wakati wa ´Aswr kwa sababu tu fulani amesema kadhaa na kadhaa. Mmoja wao akitaka kuswali mapema wanaenda na kuswali pamoja na fulani na mwingine akitaka kuchelewesha swalah wanaenda na kuswali pamoja na fulani! Lakini hapa kwetu – himdi zote ni za Allaah – katika nchi hii na chini ya kivuli cha Da´wah hii iliyobarikiwa wamerudi katika yale waliyokuwemo Salaf-us-Swaalih ambapo wanaswali pamoja na kwa wakati mmoja na nyuma ya imamu mmoja.

Mzungumzaji: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
Chanzo: Sharh Usuwl-is-Sittah
Tarehe: 11-11-2017
Mfasiri: Wanachuoni.com


  • Kitengo: Uncategorized , Faida Mbalimbali
  • Mfasiri: http://wanachuoni.com
  • Imechapishwa: Saturday 11th, November 2017