Hakuna Ahl-us-Sunnah Yeyote Aliyepinga Kuonekana Kwa Allaah Siku Ya Qiyaamah

Swali:
Kutofautiana baadhi katika masuala ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumuona Mola Wake kama ilikuwa kwa macho au kwa moyo wake ni dalili inayoonesha kuwa Maswahabah walitofautiana katika ´Aqiydah?

Jibu:

Hapana. Hawakutofautiana katika ´Aqiydah. Walitofautiana katika masuala maalum. Ama ´Aqiydah kuhusu kwamba Allaah Ataonekana siku ya Qiyaamah hawakutofautiana. Waislamu watamuona kwa macho yao. Je, kuna yeyote katika Ahl-us-Sunnah aliyepinga hili? Hakuna aliyepinga hili. Walichotofautiana ni kama alimuona kabla ya kufa (´alayhis-Swalaat was-Salaam), wakati alipokuwa bado yuhai, kwa sababu hakuna yeyote atayemuona Allaah duniani. Hakuna yeyote atayemuona Allaah duniani. Hakuna yeyote anayeweza kumuona Allaah duniani. Hili ni hata kwa Muusa (´alayhis-Salaam):

قَالَ رَبِّ أَرِنِي أَنظُرْ إِلَيْكَ ۚ قَالَ لَن تَرَانِي وَلَـٰكِنِ انظُرْ إِلَى الْجَبَلِ فَإِنِ اسْتَقَرَّ مَكَانَهُ فَسَوْفَ تَرَانِي ۚ فَلَمَّا تَجَلَّىٰ رَبُّهُ لِلْجَبَلِ جَعَلَهُ دَكًّا
”Akasema: “Mola wangu! Nionyeshe ili nikutazame.” (Allaah) Akasema: “Hutoniona! Lakini tazama jabali. Likitulia mahali pake, basi utaniona.” Basi Mola wako Alipojidhihirisha katika jabali, Alilijaalia kuwa lenye kuvurugika vurugika.” (07:143)

Jibali lilivurugika na likawa chenga chenga kutokana na ukubwa wa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Hakuna yeyote anayeweza kumuona Allaah duniani. Kuhusu Aakhirah Allaah Atawapa nguvu na Atawakirimu wamuone ili macho yao yaweze kuburudika. Wale waliomuamini duniani ilihali hawajamuona, Allaah (Jalla wa ´Alaa) Atawakirimu siku ya Qiyaamah waweze kumuona kwa macho yao ikiwa ni ikram kwao. Ama makafiri ambao walimkanusha Allaah, Allaah Atawazuia wasimuone siku ya Qiyaamah:

كَلَّا إِنَّهُمْ عَن رَّبِّهِمْ يَوْمَئِذٍ لَّمَحْجُوبُونَ
“Hapana! Hakika wao siku hiyo watawekewa kizuizi (wasimuone) Mola wao.” (83:15)

Kwa kuwa hawakumuamini Allaah (´Azza wa Jalla) duniani. Hivyo Allaah Atawazuia wasimuone na Atawanyima Pepo Yake.