Da´wah yetu


Hakika Da´wah yetu tunalingania katika yafuatayo:

Tafsiyah (kusafisha) itikadi na fikra mbalimbali zilizoenea kwa waislamu, na khaswa kwa wakati huu, ili watu wote waweze kukusanyika katika yale yaliyowakusanya waislamu wa mwanzo, nalo si jengine bali ni ´Aqiydah na mfumo sahihi. Kwa haya tunamaanisha kusafisha yale madhambi makubwa kama shirki, kufuru na Bid´ah, ikiwa vilevile ni pamoja na ufuataji kipofu wa makundi mbalimbali na maimamu na kusafisha viwiliwili na mioyo kutokamana na madhambi.

Tarbiyah (mafundisho na malezi) katika ufahamu sahihi wa Qur-aan na Sunnah – maana yake ni mtu kurejea katika ufahamu wa Salaf-us-Swaalih (wema waliotangulia) katika matukio yote. Hapo ndipo tutakuwa na imani sahihi na dalili ya hilo ni Kauli ya Allaah (Ta´ala):

وَمَن يُشَاقِقِ الرَّسُولَ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ الْهُدَىٰ وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ نُوَلِّهِ مَا تَوَلَّىٰ وَنُصْلِهِ جَهَنَّمَ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا

“Atakayempinga Mtume baada ya kuwa imeshambainikia uongofu na akaifuata njia isiyokuwa ya waumini, basi Tutamgeuza alikogeukia na tutamuingiza Motoni – na uovu ulioje mahali pa kurejea.” (an-Nisaa´ 04:115)

Waumini wanaokusudiwa hapa, kama walivyofasiri wanachuoni maimamu na wanachuoni wa tafsiri za Qur-aan, ni Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na (Radhiya Allaahu ´anhum), ambao ndio karne ya kwanza ya Salaf-us-Swaalih. Kwa hivyo, ni wajibu kuwa na imani moja kama aliyokuwa nayo Mtume na Maswahabah. Haya ndio ambayo wanachuoni wanalingania kwayo.

Swalah na salaam zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake na kila atakayewafuata kwa wema hadi siku ya Mwisho.